Skip to main content
Yanga SC

Ligi Kuu Bara Yanga yakaa sawa, yaipiga Ndanda 4-0.

YANGA jana ilijiongezea pointi tatu muhimu baada ya kuifunga Ndanda Fc mabao 4-0 katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Ushindi huo umekuja baada ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu kutoka sare ya bao 1-1 na African Lyon katika mechi iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita na hivyo kupunguzwa kasi ya kuelekea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, nafasi inayoshikiliwa na Simba.

Yanga sasa imefikisha pointi 40, ikiwa nyuma kwa pointi moja dhidi ya Simba, ikiombea Simba ipate sare ama ipoteze dhidi ya Ruvu Shooting leo ili shughuli ya kufukuzia kilele cha msimamo inoge vizuri.

Yanga ilianza mechi hiyo kwa kasi ilikishambulia lango la Ndanda na dakika ya tatu Donald Ngoma aliandika bao la kuongoza baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona wa Haruna Niyonzima.

Kuingia kwa bao hilo kuliifanya Ndanda kufurukuta kidogo ambapo katika dakika ya 12 nusura mchezaji wa zamani wa Yanga, Kigi Makasi aandike bao la kusawazisha kwa mkwaju mkali wa adhabu ndogo lakini uliishia mikononi mwa kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’.

Dakika ya 20, Ngoma aliiongezea Yanga bao la pili kwa kuunganisha krosi ya Juma Abdul kabla ya kuujaza mpira wavuni akiwaacha mabeki wa Ndanda wamezubaa wakidhani mfungaji ameotea.

Dakika tano baadae, Yanga ilipata bao la tatu lililofungwa mshambuliaji wake Amisi Tambwe baada ya kugongeana vema pasi na Ngoma kabla ya kumgeukia kipa wa Ndanda na kuujaza mpira wavuni. Baada ya bao hilo, mpira ulilazimika kusimama kwa dakika chache kutokana na kipa wa Ndanda Jeremiah Kisubi kuumia.

Mabingwa hao watetezi ambao jana walionyesha soka safi walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 3-0 kabla ya Vincent Bossou hajafunga bao la nne katika dakika 88 akiunganisha kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na Abdul.

Kwenye uwanja wa Manungu, Turiani wenyeji Mtibwa Sugar waliitambia Majimaji kwa kuifunga bao 1-0. Kwa matokeo hayo, Mtibwa imepanda mpaka nafasi ya tatu ikiwa na pointi 30 na Majimaji inabaki nafasi ya 14 na pointi zake 17.

Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Vincent Bossou, Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’/ Justine Zulu, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Emmanuel Martin/ Geoffrey Mwashiuya.

Ndanda FC: Jeremiah Kisubi/, Kiggi Makassi, Bakari Mtama, Paul Ngalema, Hemed Khoja, Salvatory Ntebe/Ayoub Shaaban, Abuu Ubwa/Salum Minely, Nassor Kapaman, Salum Telela, Omar Mponda na Riffat Khamis.

Add new comment

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Lines and paragraphs break automatically.
  • Web page addresses and email addresses turn into links automatically.