Skip to main content
Simba SC, Ruvu Shooting

Ligi Kuu Bara, Simba kuvaana na Ruvu Shooting.

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Simba leo watakuwa kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kucheza na Ruvu Shooting katika mechi inayotarajiwa kuwa ya kuvuta nikuvute.

Mechi hiyo ambayo Simba ipo ugenini, inatarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake huku mashabiki wa soka wakitamani kuona mwenendo wa Simba kama utaendelea au utaishia njiani kama ilivyo kawaida yake katika misimu iliyopita kufanya vizuri na kuvurunda mwishoni.

Presha kubwa inatarajiwa kuonekana kwa wachezaji wa Simba leo, hasa baada ya watani wao wa jadi Yanga kushinda dhidi ya Ndanda jana na hivyo kupunguza pengo la pointi.

Simba ina pointi 41 kileleni mwa msimamo na ushindi wa jana uliifanya Yanga kuisogelea kwa karibu ikiwa na pointi 40, hivyo ni ushindi pekee ndio utaihakikishia Simba kutawala kwa raha kileleni mwa msimamo huo.

Baada ya mechi hizi za raundi ya 18, ligi itasimama kupisha michuano ya kombe la Mapinduzi na itaendelea tena Januari katikati. Kocha wa Simba, Joseph Omog alisema hana wasiwasi na timu yake kwani ameiandaa kupambana na timu yoyote na kuibuka na ushindi.

“Simba msimu huu lengo lake ni ubingwa na ina kila sababu ya kuuchukua, kila mechi iliyo mbele yetu ni fainali na ndivyo itakavyokuwa kesho (leo) dhidi ya wapinzani wetu,” alisema.

Omog alisema anafahamu ugumu wa mechi zake hasa baada ya kuongoza msimamo lakini hilo halimtishi.

“Kwa vile tunaongoza sasa kila timu itataka kutufunga, lakini na sisi tumejipanga pia kuhakikisha hatuachi pointi,” alisema.

Kwa upande wa Ruvu Shooting iko nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 23. Kocha wake Malale Hamsini alisema hawaiogopi Simba bali wanaiheshimu na anaimani atapata matokeo mazuri leo.

“Simba wana timu nzuri lakini hata mimi pia timu yangu nzuri, na hatuko kwenye nafasi mbaya sana, tunataka kushinda ili tusogee juu kwenye msimamo kwa hiyo wenzetu wasidhani kwamba watatufuga kirahisi,” alisema.

Mechi nyingine leo ni kati ya Azam itakayokuwa kwenye uwanja wake Azam Complex Chamazi kumenyana na Prisons Mbeya. Azam inashika nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 27 na Prisons ni ya nane ikiwa na pointi 22.

Add new comment

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Lines and paragraphs break automatically.
  • Web page addresses and email addresses turn into links automatically.