The Sound Of Africa
Saturday May 19th 2012

Interesting Sites

Insider

Archives

WHO yataka bajeti ya utafiti iongezwe.

Na Nickson Mkilanya,

Morogoro

 

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limeziagiza nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki kutenga bajeti ya kutosha kuwawezesha watafiti wachanga kukua katika tasnia hiyo na kufanya tafiti zitakazowasaidia kukomesha usugu wa magonjwa katika nchi zao.

Kaimu Mwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni nchini Dokta Lita Njau ametoa agizo hilo wakati wa ufunguzi wa semina ya watafiti na wanasayansi kutoka nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki inayoendelea katika chuo kikuu cha Kilimo cha sokoine SUA.

Katika semina hiyo ya wiki mbili inayoangalia usugu wa magonjwa na dawa mbadala kwa magonjwa ambayo yameonekana kuwa sugu katika nchi za Bara la Afrika, Dokta Njau amesema ni kwa njia ya wanasayansi na watafiti kupewa fedha za kutosha za kuendeshea tafiti zao ndiko kutasaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa matatizo ya magonjwa sugu.

Kiongozi mwandamizi wa maabara ya kudhibiti malaria kutoka nchini Marekani Dokta Patrick Duffy amesema nchi yake inalenga kuona idadi ya watoto na watu wazima wanaougua ugonjwa wa Malaria katika Bara la Afrika inapungua.

Naye kiongozi wa mradi wa kudhibiti Malaria kwa watoto wachanga na wanawake wajawazito kutoka SUA Profesa Paul Gwakisa amesema mradi huo umepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake na kwamba wapo katika hatua za kupata sehemu ya chanjo ya ugonjwa wa Malaria.

Mtafiti kutoka taasisi ya taifa ya Utafiti Dokta Hamisi Malebo ameeleza sababu za kubadilishwa kwa dawa za ugonjwa wa malaria mara kwa mara kuwa ni kutokana na matumizi yasiyozingatia maelekezo sahihi ya dawa wakati ambapo Wanasayansi kutoka Kenya na Uganda wameeleza faida za wanataaluma kukutanishwa pamoja kuwa ni kuwa na nguvu za pamoja za kupambana na Magonjwa sugu.

Mradi huo wa kitafiti ambao umetimiza miaka 10 mwaka huu, umekuwa ukishirikisha tafiti za magonjwa mbalimbali ya binadamu ikiwamo Malaria na Kifua Kikuu sanjari na kutafuta dawa mbadala pale dawa moja inaposhindwa kutibu ugonjwa husika.

Mwisho

Related posts:

Related Ways to Take Action:
Powered by Social Actions

Leave a Reply