Na Joachim Nyambo,Mbeya
MEYA wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga ametaka busara zitumike
kumshauri Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuri kuachana na mpango wake
wa kuvunja mabango ya matangazo yaliyo kando ya barabara katika miji,
Manispaa na majiji nchini kote.
Akizungumza na RFA, Kapunga amesema suala hilo hivi sasa ni la
kitaifa, halipaswi kushughulikiwa na mtu mmoja mmoja badala yake
akawataka wakurugenzi, mameya na wenyeviti wa halmashauri kuungana
pamoja na kutumia busara kumvaa Dk. Magufuri ili aweze kuachana na
mpango wake wa kuyaondoa mabango hayo.
Akifafanua zaidi, Meya Kapunga amesema mabango hayo yanaziingizia
halmashauri fedha ambazo zinaingizwa kwenye bajeti ya Halmashauri na
kupelekwa kwemye miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.
Kapunga ambaye pia ni Diwani wa Itiji Jijini Mbeya alisema madai ya
Waziri Magufuri kuwa fedha hizo zinatumika kwa madiwani kugawana posho
sio ya kweli na badala yake fedha hizo huingizwa kwenye bajeti na
kutumika kwa manufaa ya wananshi na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo Kapunga amesema ikiwa Serikali itayaondoa mabango hayo kwa
nia ya kutaka kupanua barabara, yeye hana kipingamizi, lakini kwa kuwa
muda wa upanuzi wa barabara haujafika anaona ni vema mabango hayo
yakaachwa ili yaendelee kuziingizia mapato halmashauri.
Naye Diwani wa kata ya Mwakibete Jijini Mbeya, Lucas Mwampiki
(Chadema) amesema fedha zinazopatikana kutokana na mabango hayo
zinatumika kwa manufaa ya Halmashauri na kudai kuwa Dk. Magufuri
alikurupuka kwa kusema kuwa madiwani hutumia fedha hizo kwa kugawana
posho.
Amesema Dk. Magufuri ametoa kauli hiyo bila kufanya utafiti wa aina ya
vyanzo vya mapato ya halmashauri na jinsi halmashauri husika
zinavyotumia fedha zitokanazo na mapato yake.
Amesema viwango vya posho za madiwani kwa mwezi zinajulikana kuwa ni
shilingi 120,000 hivyo hata kama mabango hayo yataondolewa badho posho
hizo bado zitalipwa.
Mwampiki amesema fedha zinazoingia kwenye halmashauri kwa kukusanya
ushuru wa mabango, zinafanya kazi za kijamii kama vile kujenga shule,
zahanati na kutoa misaada kwa watu wa makundi maalum na kamwe
hazitumiki kwa kunufaisha madiwani.
Hivi karibuni, Waziri wa Magufuri alisisitiza msimamo wake wa
kuyaondoa mabango yote yaliyowekwa kwenye hifadhi ya barabara akidai
kuwa anatekeleza sheria na kamwe hakuna mtu wa kumsaidia.
Mwisho.










