Na Mwandishi Maalum, Kilimanjaro.
MGOMBEA urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa barabara zote kuu nchini zitakuwa zimewekewa lami katika miaka mitano ijayo kama atachaguliwa tena kuongoza Tanzania.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa kuanzia mwakani kila mwanafunzi wa sekondari nchini atakuwa na kitabu chake cha masomo ya sayansi ikiwamo hisabati.
Vile vile, mgombea huyo wa CCM amesisitiza kuwa ahadi zinazotolewa na chama hicho na wagombea wake wakati wa Kampeni ya sasa ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu siyo za kutaka chama hicho na wagombea wake wapewe kura bali ni ahadi ambazo zimefanyiwa kazi.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Jumatano, Septemba 15, 2010, wakati alipohutubia mikutano ya Kampeni ya Uchaguzi Mkuu katika majimbo ya Rombo, Vunjo na Moshi Mjini katika Mkoa wa Kilimanjaro ambako mgombea huyo wa CCM amepokelewa na moja ya umati mkubwa zaidi uliopata kujitokeza kumsikiliza tokea aanze Kampeni yake Agosti 21, mwaka huu.
Akihutubia maelfu kwa maelfu ya wananchi katika Uwanja wa Mashujaa mjini Moshi jioni ya leo, Rais Kikwete amefafanua kwa ufasaha Ilani ya CCM kuhusu jinsi CCM inavyozielekeza Serikali zake kujenga barabara nchini na azama yake mwenyewe kuhusu ujenzi wa barabara hizo endapo atachaguliwa tena kuwa Rais wa Tanzania.
“Ilani inatuelekeza vizuri kuhusu ujenzi wa barabara, na mimi nataka kuhakikisha kuwa barabara zote kuu nchini zinajengwa kwa kiwango cha lami katika miaka mitano ijayo,” Rais Kikwete amewaambia maelfu kwa maelfu ya wananchi waliokuwa wakimshangilia kwa nguvu kwenye Uwanja wa Mashujaa.
Rais pia amefafanua mipango ya Serikali yake kupambana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kama atachaguliwa tena kuwa Rais.
Changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa walimu, ukosefu wa vitabu kwa wanafunzi, uhaba wa nyumba za walimu na ukosefu wa maabara.
Mheshimiwa Kikwete ameeleza kuwa Serikali ya Marekani imeanza kutekeleza azma yake ya kusaidia kuichapishia Tanzania vitabu vya hisabati, fizikia, kemia na biolojia kama ambavyo marais Georbe Bush na Barack Obama walimwahidi Rais Kikwete kwa nyakati tofauti wakati viongozi hao wa Marekani walipokutana na Rais Kikwete.
Amesema kuwa tayari Serikali ya Marekani imekwishaikabidhi Tanzania vitabu 800,000 na ifikapo mwanzoni mwa mwaka ujao, Tanzania itakabidhiwa vitabu vingine 2.5 milioni na hivyo kumaliza tatizo hilo la vitabu vya sayansi kwa wanafunzi wa sekondari nchini.
“Kuanzia mwakani, tuna hakika kuwa kila mwanafunzi wa shule ya sekondari nchini atakuwa na kitabu chake cha hisabati, fikizia, kemia na biolojia.
Changamoto hii tunaifikisha mwisho katika jitihada zetu kuboresha elimu ya watoto wetu nchini,” amesema Rais Kikwete.
Kuhusu uhaba wa walimu katika shule za sekondari nchini, Rais Kikwete amesema kuwa safari ya kumaliza tatizo hilo nayo imeanza na kuwa vyuo vikuu vya Tanzania na vile vya ualimu vitatoa walimu wasiopungua 19,000 mwaka huu.
Amesema kuwa kuanzia mwakani, kila shule ya sekondari ya kata nchini itapatiwa wastani wa walimu watano wapya kila mwaka kutokana na ongezeko hilo kubwa la walimu wapya.
Kuhusu maabara, Rais Kikwete amesema kuwa tayari Serikali imepata mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya kujenga maabara katika shule zote za kata nchini na kuwa Serikali itajenga nyumba za walimu kwa kutumia raslimali zake yenyewe.
Kuhusu ahadi ambazo zimekuwa zinatolewa na Chama cha Mapinduzi na wagombea wake wa nafasi mbali mbali akiwamo yeye mwenyewe, Rais Kikwete amesema kuwa CCM na wagombea wake hawatoi ahadi hewa.
“Hatutoi ahadi hewa kwa sababu ya kutaka tu tupigiwe kura. Hapana. Ahadi zetu ni kutokana na mambo ambayo tumeyafikiria, tumeyatafakari na tumeyafanyia uamuzi.
Chetu ni chama makini, kinayajua mambo ya msingi nchini na kinayafanyia kazi vizuri kabla ya kuyaweka hadharani.”
Leo, mgombea huyo wa urais wa CCM amefanya mikutano na kampeni na kusalimia wananchi katika maeneo ya Rombo-Tarakea, Robo-Mashati, Mkuu, Mengwe, Mwika, Himo, Marangu Mtoni, Kilema, Kirua-Vunjo, na Moshi Mjini.
Kesho,Alhamisi, Septemba 16, 2010, Rais Kikwete anaendelea na Kampeni zake katika majimbo ya Siha na Hai ya Mkoa wa Kilimanjaro kabla ya kuingia katika Mkoa wa Arusha.










